Wagalatia 3:15-29
Wagalatia 3:15-29 SRUV
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazawa, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa njia ya ahadi. Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hadi aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki. Hakuna mtumwa wala huru. Hakuna mwanamume wala mwanamke. Maana ninyi nyote mmekuwa wamoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Abrahamu, na warithi kulingana na ahadi.