Kutoka 29:29-46
Kutoka 29:29-46 Biblia Habari Njema (BHN)
“Baada ya kufa kwake Aroni, mavazi yake matakatifu yatakabidhiwa wazawa wake, nao watayavaa siku yao ya kupakwa mafuta na kuwekewa mikono. Mwana wa Aroni atakayekuwa kuhani mahali pa baba yake atayavaa mavazi hayo siku saba katika hema la mkutano, ili kuhudumu katika mahali patakatifu. “Utachukua nyama ya huyo kondoo wa kuwaweka wakfu na kuichemshia katika mahali patakatifu. Kisha utawapa Aroni na wanawe, nao wataila mlangoni pa hema la mkutano pamoja na ile mikate iliyosalia kapuni. Watavila vitu hivyo vilivyotumika kuwaweka wakfu na kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho, lakini mtu mwingine asiruhusiwe kuvila kwani ni vitakatifu. Kama nyama yoyote au mikate hiyo itasalia mpaka asubuhi yake, basi utaiteketeza kwa moto; isiliwe maana ni kitu kitakatifu. “Hivyo ndivyo utakavyowatendea Aroni na wanawe kufuatana na yote yale niliyokuamuru; utawaweka wakfu kwa muda wa siku saba, na kila siku utatoa fahali awe sadaka ya kuondolea dhambi ili kufanya upatanisho, na kwa kufanya hivyo utaitakasa madhabahu; kisha utaimiminia mafuta ili kuiweka wakfu. Kwa siku saba utaifanyia madhabahu upatanisho na kuiweka wakfu. Baada ya hayo, madhabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kila siku, wakati wote ujao, utatolea sadaka juu ya madhabahu: Wanakondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Mwanakondoo mmoja utamtoa sadaka asubuhi na mwingine jioni. Pamoja na mwanakondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na lita moja ya mafuta safi, na lita moja ya divai kama sadaka ya kinywaji. Hali kadhalika na yule mwanakondoo mwingine wa jioni utamtolea tambiko pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji kama ulivyofanya asubuhi; harufu ya tambiko hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa daima, kizazi hata kizazi, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, mbele ya mlango wa hema la mkutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi. Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu. Hema la mkutano na madhabahu nitavifanya vitakatifu; vilevile Aroni na wanawe nitawaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani. Nitaishi kati ya Waisraeli, nami nitakuwa Mungu wao. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili niishi kati yao. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
Kutoka 29:29-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu. Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu. Nawe twaa huyo kondoo dume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. Na kwamba kitu chochote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au chochote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu. Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba. Kila siku utamtoa ng'ombe dume wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa. Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja kila siku. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yaliyopondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, na utamtoa dhabihu pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji kama asubuhi, ili itoe harufu nzuri, iwe dhabihu ya kusogeswa kwa Bwana kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. Nao watanijua kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, niliyewatoa katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi BWANA Mungu wao.
Kutoka 29:29-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu. Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu. Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu. Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba. Kila siku utamtoa ng’ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa. Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. Nao watanijua kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi BWANA Mungu wao.
Kutoka 29:29-46 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wazao wake ili waweze kupakwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa. Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba. “Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu. Haruni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania. Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu. Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki hadi asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu. “Hivyo utamfanyia Haruni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu. Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uipake mafuta na kuiweka wakfu. Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni. Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. “Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za BWANA. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi, Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu. “Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Haruni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani. Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao. Nao watajua kuwa Mimi Ndimi BWANA Mungu wao, aliyewatoa Misri ili nipate kufanya makao miongoni mwao. Mimi Ndimi BWANA Mungu wao.