Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 29:29-46

Kutoka 29:29-46 SRUV

Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu. Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu. Nawe twaa huyo kondoo dume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. Na kwamba kitu chochote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au chochote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu. Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba. Kila siku utamtoa ng'ombe dume wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa. Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja kila siku. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yaliyopondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, na utamtoa dhabihu pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji kama asubuhi, ili itoe harufu nzuri, iwe dhabihu ya kusogeswa kwa Bwana kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. Nao watanijua kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, niliyewatoa katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi BWANA Mungu wao.

Soma Kutoka 29