Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 29

29
Kuweka wakfu makuhani
(Walawi 8:1-36)
1“Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari. 2Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate myembamba iliyopakwa mafuta. 3Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili. 4Kisha mlete Haruni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. 5Chukua yale mavazi na umvike Haruni koti, joho la kizibau, na kizibau chenyewe, pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kizibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi. 6Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu lishikamane na hicho kilemba. 7Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake. 8Walete wanawe na uwavike makoti, 9pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Haruni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Haruni na wanawe.
10“Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. 11Mchinje huyo fahali mbele za Mwenyezi Mungu kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 12Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu. 13Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu. 14Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi.
15“Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. 16Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu. 17Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine. 18Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
19“Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Haruni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. 20Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Haruni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu. 21Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Haruni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Haruni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu.
22“Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.) 23Kutoka kwa kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Mwenyezi Mungu, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta, na mkate mwembamba. 24Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe na uviinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. 25Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Mwenyezi Mungu, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. 26Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Haruni, kiinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako.
27“Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Haruni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. 28Siku zote hili litakuwa fungu la milele kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Haruni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Mwenyezi Mungu kutoka sadaka zao za amani.
29“Mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wazao wake ili waweze kupakwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa. 30Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba.
31“Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu. 32Haruni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania. 33Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu. 34Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki hadi asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu.
35“Hivyo utamfanyia Haruni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu. 36Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uipake mafuta na kuiweka wakfu. 37Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
38“Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. 39Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni. 40Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja#29:40 Efa moja ni sawa na kilo 22. ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini#29:40 Robo ya hini ni sawa na lita moja. ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. 41Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
42“Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi, 43Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu.
44“Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Haruni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani. 45Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao. 46Nao watajua kuwa Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewatoa Misri ili nipate kufanya makao miongoni mwao. Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 29: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia