Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 30

30
Madhabahu ya kufukizia uvumba
(Kutoka 37:25-28)
1“Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba. 2Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja#30:2 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45., na kimo cha dhiraa mbili#30:2 Dhiraa mbili ni sawa na sentimita 90., nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo. 3Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka. 4Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu. 5Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu. 6Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la ule Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ule Ushuhuda, mahali nitakapokutana nawe.
7“Itampasa Haruni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa. 8Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Mwenyezi Mungu kwa vizazi vijavyo. 9Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake. 10Mara moja kwa mwaka Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Mwenyezi Mungu.”
Fedha ya upatanisho
11Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 12“Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Mwenyezi Mungu fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu. 13Kila mmoja anayeenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli#30:13 Nusu shekeli ni sawa na gramu 6., kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini#30:13 Gera 20 ni sawa na shekeli moja au gramu 12.. Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Mwenyezi Mungu. 14Wote wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu. 15Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu. 16Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”
Sinia la kunawia
17Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 18“Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. 19Haruni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji ya hilo sinia. 20Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, 21watanawa mikono na miguu yao ili wasije wakafa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Haruni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”
Mafuta ya upako
22Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 23“Chukua vikolezo bora vifuatavyo: shekeli mia tano#30:23 Shekeli 500 ni sawa na kilo 6. za manemane ya maji, shekeli mia mbili na hamsini#30:23 Shekeli 250 ni sawa na kilo 3. za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli mia mbili na hamsini za miwa yenye harufu nzuri, 24shekeli mia tano za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini#30:24 Hini moja ni sawa na lita 4. ya mafuta ya zeituni. 25Vitengeneze vikolezo hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. 26Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, 27meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 28madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. 29Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
30“Mpake Haruni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 31Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. 32Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. 33Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na kuyamimina juu ya mtu ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”
Uvumba
34Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chukua vikolezo vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, 35pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. 36Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali nitakapokutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. 37Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu. 38Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 30: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia