Kutoka 13:17-22
Kutoka 13:17-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati Farao alipowaachia Waisraeli waende zao, Mungu hakuwapitisha katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa ya karibu. Mungu alisema, “Sipendi watu hawa wabadilishe nia na kurudi Misri wakijua itawabidi kupigana vita.” Badala yake, Mungu aliwapitisha Waisraeli katika njia ya mzunguko kupitia jangwani, kuelekea bahari ya Shamu. Waisraeli waliondoka nchini Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita. Mose aliichukua mifupa ya Yosefu kama Yosefu alivyoagiza kabla ya kufa kwake. Alikuwa amewaapisha rasmi Waisraeli akisema, “Mungu atakapowajia kuwatoa nchini humu, ni lazima mwichukue mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.” Basi, Waisraeli waliondoka Sukothi, wakapiga kambi huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa. Mchana Mwenyezi-Mungu aliwatangulia katika mnara wa wingu kuwaonesha njia, na usiku aliwatangulia katika mnara wa moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana na usiku. Mnara wa wingu wakati wa mchana, na mnara wa moto wakati wa usiku, kamwe haikukosekana kuwatangulia Waisraeli.
Kutoka 13:17-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ilikuwa hapo Farao alipowaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakabadili nia watu hawa hapo watakapokumbana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri wakiwa tayari kwa vita. Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi. Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa lile jangwa. BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.
Kutoka 13:17-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi. Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa. BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.
Kutoka 13:17-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitiayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.” Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita. Mose akachukua mifupa ya Yosefu kwa sababu Yosefu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwiichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.” Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa. Wakati wa mchana BWANA aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku. Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.