Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 13

13
Kuwaweka wakfu wazaliwa wa kwanza
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Niwekee wakfu wazaliwa wote wa kwanza wa kiume, maana wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa Waisraeli na kila wazaliwa wa kwanza wa wanyama ni wangu.”
Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu
3Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii mliyotoka nchini Misri ambako mlikuwa watumwa. Hii ndiyo siku Mwenyezi-Mungu alipowatoa humo kwa mkono wake wenye nguvu. Katika siku hii, kamwe msile mkate uliotiwa chachu. 4Siku hii, mwezi wa kwanza wa Abibu, mtaondoka nchini Misri. 5Na wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi ambayo aliwaapia babu zenu kwamba atawapa nyinyi, nchi inayotiririka maziwa na asali, ni lazima muiadhimishe sikukuu hii kila mwaka katika mwezi huu wa kwanza. 6Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, na mnamo siku ya saba mtafanya sikukuu kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. 7Kwa muda huo wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Kusiwepo na mikate iliyotiwa chachu, wala chachu yoyote miongoni mwenu na katika nchi yenu yote. 8Siku hiyo mtawaambia watoto wenu kwamba mnafanya hivyo kwa sababu ya jambo alilowafanyia Mwenyezi-Mungu mlipoondoka nchini Misri. 9Adhimisho hilo litakuwa ukumbusho, kama alama katika mikono yenu au katika paji la nyuso zenu; ili iwakumbushe daima sheria ya Mwenyezi-Mungu. Maana, Mwenyezi-Mungu amewatoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu. 10Kwa hiyo, mtaadhimisha sikukuu hii kwa wakati uliopangwa, kila mwaka.”
Maelezo kuhusu wazaliwa wa kwanza
11Mose akaendelea kuwaambia watu, “Hali kadhalika, wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani na kuwapeni iwe mali yenu kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu, 12#Taz Kut 34:19-20; Luka 2:23 lazima kumwekea Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yenu atakuwa wa Mwenyezi-Mungu. 13Lakini mzaliwa wa kwanza wa kiume wa punda utamkomboa kwa kulipa mwanakondoo, la sivyo, utamuua kwa kumvunja shingo. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa binadamu utamkomboa. 14Kama hapo baadaye mwanao akiuliza maana ya jambo hili, utamwambia, ‘Kwa nguvu ya mkono wake, Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri ambako tulikuwa watumwa. 15Farao kwa ukaidi alikataa kutuachia tuondoke; kwa hiyo Mwenyezi-Mungu alimuua kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri, mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa mnyama. Basi, mimi ninamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yangu, lakini kila mzaliwa wa kwanza wa wanangu namkomboa.’ 16Jambo hili litakuwa kama alama mkononi mwako au utepe katika paji la uso wako, kwamba Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu.”
Mnara wa wingu na wa moto
17Wakati Farao alipowaachia Waisraeli waende zao, Mungu hakuwapitisha katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa ya karibu. Mungu alisema, “Sipendi watu hawa wabadilishe nia na kurudi Misri wakijua itawabidi kupigana vita.” 18Badala yake, Mungu aliwapitisha Waisraeli katika njia ya mzunguko kupitia jangwani, kuelekea bahari ya Shamu.#13:18 bahari ya Shamu: Kiebrania neno kwa neno ni “bahari ya mafunjo”. Waisraeli waliondoka nchini Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.
19 # Taz Mwa 50:25; Yos 24:32 Mose aliichukua mifupa ya Yosefu kama Yosefu alivyoagiza kabla ya kufa kwake. Alikuwa amewaapisha rasmi Waisraeli akisema, “Mungu atakapowajia kuwatoa nchini humu, ni lazima mwichukue mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.”
20Basi, Waisraeli waliondoka Sukothi, wakapiga kambi huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa. 21Mchana Mwenyezi-Mungu aliwatangulia katika mnara wa wingu kuwaonesha njia, na usiku aliwatangulia katika mnara wa moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana na usiku. 22#Taz Hek 10:17-18; 18:3 Mnara wa wingu wakati wa mchana, na mnara wa moto wakati wa usiku, kamwe haikukosekana kuwatangulia Waisraeli.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 13: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha