Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 7:1-10

Esta 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Hivyo mfalme na Hamani wakaenda kula karamu na malkia Esta. Katika siku ya pili, walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta, “Sasa, malkia Esta, unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Malkia Esta akamjibu, “Kama nimepata upendeleo kwako, ewe mfalme, na ukiwa radhi kunitimizia ombi langu, haja yangu ni mimi niishi na watu wangu pia. Maana, mimi na watu wangu tumeuzwa tuuawe, kuangamizwa na kufutiliwa mbali. Kama tungeuzwa tu kuwa watumwa na watumwa wa kike, ningekaa kimya, wala nisingekusumbua. Ingawa tutakatiliwa mbali hakuna adui atakayeweza kufidia hasara hii kwa mfalme.” Hapo mfalme Ahasuero akamwuliza malkia Esta, “Ni nani huyo athubutuye kufanya jambo kama hilo? Yuko wapi mtu huyo?” Esta akamjibu, “Adui yetu mkuu na mtesi wetu, ni huyu mwovu Hamani!” Hapo Hamani akashikwa na hofu mbele ya malkia na mfalme. Mfalme akasimama kwa hasira, akatoka chumbani kwenye karamu ya divai na kwenda nje kwenye bustani ya ikulu. Hamani alipoona kwamba mfalme amenuia kumwadhibu, alibaki nyuma kumsihi malkia Esta ayasalimishe maisha yake. Baadaye mfalme alirudi kutoka bustanini, na mara alipoingia chumbani walimokuwa wanakunywa divai, alimkuta Hamani amejitupa karibu na kochi ambamo Esta alikuwa amekaa. Kuona hivyo, mfalme alisema kwa sauti kuu, “Hivi mtu huyu anataka kumshika kwa nguvu malkia mbele yangu, tena ndani ya ikulu?” Mara kabla mfalme hajamaliza kusema, matowashi wakamfunika Hamani uso. Harbona, mmoja wa wale matowashi waliomhudumia mfalme, akasema, “Hamani amethubutu hata kutengeneza mti wa kumwulia Mordekai ambaye aliyaokoa maisha yako, ewe mfalme. Mti huo, wenye urefu wa mita ishirini na mbili, bado uko huko nyumbani kwake.” Hapo mfalme akaamuru, “Mwulie Hamani papo hapo.” Naye, Hamani akauawa hapo kwenye mti wa kuulia aliokuwa amemtayarishia Mordekai. Basi, hasira ya mfalme ikapoa.

Shirikisha
Soma Esta 7

Esta 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi mfalme na Hamani walikwenda kula karamu pamoja na malkia Esta. Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Ikiwa nimepata kibali machoni pako, Ewe Mfalme, na ikimpendeza mfalme, hebu nipewe maisha yangu kwa ombi langu, na watu wangu kwa maombi yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; japo hata hivyo adui asingeweza kufidia hasara ya mfalme. Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi? Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia. Mfalme akaondoka kwa ghadhabu kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme. Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hadi mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani. Ndipo aliposema Harbona, towashi mmojawapo wa wale waliohudumu mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake. Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.

Shirikisha
Soma Esta 7

Esta 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi mfalme na Hamani walikuja kula karamu pamoja na malkia Esta. Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme. Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi? Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia. Mfalme akaondoka katika ghadhabu yake kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme. Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hata mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani. Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake. Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.

Shirikisha
Soma Esta 7

Esta 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi mfalme na Hamani wakaenda kula chakula pamoja na Malkia Esta. Walipokuwa wakinywa mvinyo katika siku ya pili, mfalme akauliza tena, “Malkia Esta, ni nini haja yako? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Kisha Malkia Esta akajibu, “Kama nimepata kibali kwako, ee mfalme, tena kama inapendeza utukufu wako, nijalie maisha yangu, hii ndiyo haja yangu. Pia uokoe watu wangu, hili ndilo ombi langu. Kwa kuwa mimi na watu wangu tumeuzwa kwa kuangamizwa, kuchinjwa na kuharibiwa. Kama tungalikuwa tumeuzwa tu kuwa watumwa wa kiume na wa kike, ningalinyamaza kimya, kwa sababu shida kama hii isingalitosha kumsumbua mfalme.” Mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta, “Ni nani huyu? Yuko wapi mtu huyu aliyethubutu kufanya jambo kama hili?” Esta akasema, “Mtesi na adui ni huyu mwovu Hamani.” Hamani alifadhaika mbele ya mfalme na malkia. Mfalme akainuka kwa ghadhabu, akaacha mvinyo wake, akaenda kwenye bustani ya jumba la kifalme. Lakini Hamani, akitambua kwamba mfalme ameshaamua hatima yake, alibaki nyuma kumsihi Malkia Esta aokoe maisha yake. Mara mfalme aliporudi kutoka bustani ya jumba la kifalme na kuja kwenye ukumbi wa karamu, Hamani alikuwa akijitupa juu ya kiti mahali ambapo Esta alikuwa akiegemea. Mfalme akasema kwa nguvu, “Je, atamdhalilisha malkia hata huku nyumbani akiwa pamoja nami!” Mara neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, walifunika uso wa Hamani. Kisha Harbona, mmoja wa matowashi wanaomtumikia mfalme, akasema, “Mahali pa kuangika watu penye urefu wa mita ishirini na mbili pako nyumbani mwa Hamani. Alikuwa amepatengeneza kwa ajili ya Mordekai, ambaye alizungumza ili kumsaidia mfalme.” Mfalme akasema, “Mwangikeni juu yake!” Kwa hiyo wakamtundika Hamani mahali alipokuwa ameandaa kwa ajili ya Mordekai. Ndipo ghadhabu ya mfalme ikatulia.

Shirikisha
Soma Esta 7

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha