Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 7:1-10

Esta 7:1-10 SRUV

Basi mfalme na Hamani walikwenda kula karamu pamoja na malkia Esta. Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Ikiwa nimepata kibali machoni pako, Ewe Mfalme, na ikimpendeza mfalme, hebu nipewe maisha yangu kwa ombi langu, na watu wangu kwa maombi yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; japo hata hivyo adui asingeweza kufidia hasara ya mfalme. Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi? Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia. Mfalme akaondoka kwa ghadhabu kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme. Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hadi mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani. Ndipo aliposema Harbona, towashi mmojawapo wa wale waliohudumu mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake. Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.

Soma Esta 7

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Esta 7:1-10

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha