Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 7

7
1Hivyo mfalme na Hamani wakaenda kula karamu na malkia Esta. 2Katika siku ya pili, walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta, “Sasa, malkia Esta, unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” 3Malkia Esta akamjibu, “Kama nimepata upendeleo kwako, ewe mfalme, na ukiwa radhi kunitimizia ombi langu, haja yangu ni mimi niishi na watu wangu pia. 4Maana, mimi na watu wangu tumeuzwa tuuawe, kuangamizwa na kufutiliwa mbali. Kama tungeuzwa tu kuwa watumwa na watumwa wa kike, ningekaa kimya, wala nisingekusumbua. Ingawa tutakatiliwa mbali hakuna adui atakayeweza kufidia hasara hii kwa mfalme.”#7:4 Kiebrania si dhahiri.
5Hapo mfalme Ahasuero akamwuliza malkia Esta, “Ni nani huyo athubutuye kufanya jambo kama hilo? Yuko wapi mtu huyo?” 6Esta akamjibu, “Adui yetu mkuu na mtesi wetu, ni huyu mwovu Hamani!” Hapo Hamani akashikwa na hofu mbele ya malkia na mfalme.
7Mfalme akasimama kwa hasira, akatoka chumbani kwenye karamu ya divai na kwenda nje kwenye bustani ya ikulu. Hamani alipoona kwamba mfalme amenuia kumwadhibu, alibaki nyuma kumsihi malkia Esta ayasalimishe maisha yake. 8Baadaye mfalme alirudi kutoka bustanini, na mara alipoingia chumbani walimokuwa wanakunywa divai, alimkuta Hamani amejitupa karibu na kochi ambamo Esta alikuwa amekaa. Kuona hivyo, mfalme alisema kwa sauti kuu, “Hivi mtu huyu anataka kumshika kwa nguvu malkia mbele yangu, tena ndani ya ikulu?” Mara kabla mfalme hajamaliza kusema, matowashi wakamfunika Hamani uso. 9Harbona, mmoja wa wale matowashi waliomhudumia mfalme, akasema, “Hamani amethubutu hata kutengeneza mti wa kumwulia Mordekai ambaye aliyaokoa maisha yako, ewe mfalme. Mti huo, wenye urefu wa mita ishirini na mbili, bado uko huko nyumbani kwake.” Hapo mfalme akaamuru, “Mwulie Hamani papo hapo.” 10Naye, Hamani akauawa hapo kwenye mti wa kuulia aliokuwa amemtayarishia Mordekai. Basi, hasira ya mfalme ikapoa.

Iliyochaguliwa sasa

Esta 7: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha