Waefeso 4:1-16
Waefeso 4:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni nyinyi kwa nyinyi kwa mapendo. Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote. Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo. Kama yasemavyo Maandiko: “Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi.” Basi, inaposemwa: “Alipaa juu,” ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani. Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu. Ndiye aliyewapa watu zawadi: Wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Injili, wengine wachungaji na waalimu. Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo, na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu ili wawapotoshe wengine kwa hila. Kama tukiuzingatia ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.
Waefeso 4:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Kuna mwili mmoja, na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Waefeso 4:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Waefeso 4:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo. Kwa hiyo husema: “Alipopaa juu zaidi, aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa.” (Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia? Yeye aliyeshuka ndiye alipaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.) Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.