Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 4:1-16

Waefeso 4:1-16 NEN

Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo. Kwa hiyo husema: “Alipopaa juu zaidi, aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa.” (Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia? Yeye aliyeshuka ndiye alipaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.) Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waefeso 4:1-16