Kumbukumbu la Sheria 1:26-33
Kumbukumbu la Sheria 1:26-33 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini nyinyi hamkufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kukataa kwenda katika nchi hiyo. Mlinungunika ndani ya mahema yenu mkisema, ‘Mwenyezi-Mungu anatuchukia na ndiyo maana alitutoa nchini Misri. Alitaka kututia mikononi mwa Waamori, atuangamize. Kwa nini tuende huko hali tumevunjika moyo kwa hofu? Wametuambia kuwa watu wa huko ni wakubwa na warefu kuliko sisi, na kwamba miji yao ni mikubwa na yenye kuta zifikazo mawinguni. Tena wamesema kwamba waliwaona wale wazawa wa Anaki!’ “Lakini mimi niliwaambieni hivi: ‘Msiwe na hofu wala msiwaogope watu hao.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye huwatangulia, yeye mwenyewe atapigana kwa ajili yenu kama alivyofanya mbele yenu kule Misri na kule jangwani ambako mliona jinsi alivyowabeba safari hiyo yote kama vile baba amchukuavyo mwanawe mpaka mkafika hapa. Lakini japo nilisema hayo yote, nyinyi hamkumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatangulia njiani na kuwatafutia mahali pa kupiga kambi zenu. Usiku aliwatangulieni kwa moto na mchana kwa wingu, ili kuwaonesha njia.
Kumbukumbu la Sheria 1:26-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini hamkukubali kukwea huko, mliasi neno la BWANA, Mungu wenu; mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. Ndipo nikawaambia msiwaogope. BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafika mahali hapa. Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu, aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.
Kumbukumbu la Sheria 1:26-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la BWANA, Mungu wenu; mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. Ndipo nikawaambieni, Msifanye hofu, wala msiwache. BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa. Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu, aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonyesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.
Kumbukumbu la Sheria 1:26-33 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Mkanung’unika ndani ya mahema yenu na kusema, “Mwenyezi Mungu anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza. Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ” Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa, na pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea hadi mkafika mahali hapa.” Pamoja na hili, hamkumtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonesha njia mtakayoiendea.