Kumbukumbu la Torati 1:26-33
Kumbukumbu la Torati 1:26-33 SRUV
Lakini hamkukubali kukwea huko, mliasi neno la BWANA, Mungu wenu; mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. Ndipo nikawaambia msiwaogope. BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafika mahali hapa. Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu, aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.