2 Mambo ya Nyakati 34:19-33
2 Mambo ya Nyakati 34:19-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya torati, aliyararua mavazi yake. Mfalme akawaamuru Hilkia, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Abdoni, mwana wa Mika, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, kusema, Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa hao waliosalia wa Israeli na wa Yuda, katika habari za maneno ya kitabu kilichoonekana; maana ghadhabu ya BWANA ni nyingi iliyomwagika juu yetu, kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la BWANA, kutenda sawasawa na yote yaliyoandikwa kitabuni humo. Basi Hilkia, na hao waliotumwa na mfalme, wakamwendea Hulda nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tohathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi; (naye alikuwa akikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili); wakasema naye kama hayo. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu, BWANA asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda; kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike. Lakini mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kwa habari ya maneno uliyoyasikia, kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA. Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari. Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda mfalme nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana nyumbani mwa BWANA. Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo. Akawafanya wote walioonekana katika Yerusalemu na Benyamini walikubali. Na wenyeji wa Yerusalemu wakafanya sawasawa na agano la Mungu, Mungu wa baba zao. Naye Yosia akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi zote zilizokuwa milki ya wana wa Israeli, akawafanya wote walioonekana katika Israeli kutumika, naam, wamtumikie BWANA, Mungu wao. Siku zake zote hawakuacha kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.
2 Mambo ya Nyakati 34:19-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme aliposikia maneno ya sheria alirarua mavazi yake. Ndipo alipomwamuru Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, katibu Shafani na Asaya, mtumishi wa mfalme, akisema, “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu ambao wamebaki katika Israeli na Yuda, kuhusu maneno yaliyomo katika kitabu kilichopatikana. Kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imetuangukia, maana babu zetu hawakushika neno la Mwenyezi-Mungu, wala kufanya yaliyoandikwa humo.” Kwa hiyo Hilkia pamoja na wale wengine mfalme aliowatuma walimwendea nabii Hulda, mkewe Shalumu, mwana wa Tokathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi yaliyotumika hekaluni (alikuwa anaishi Yerusalemu katika mtaa wa pili); nao walizungumza naye juu ya mambo yaliyotokea. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambie huyo aliyewatuma kwangu, Mwenyezi-Mungu anasema hivi, ‘Tazama nitaleta uovu juu ya Yerusalemu na juu ya wakazi wake, laana zote zilizoandikwa katika kitabu kilichosomwa mbele ya mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukizia miungu mingine ubani ili wanikasirishe sana kwa kazi zote za mikono yao, basi ghadhabu yangu itamwagika juu ya mahali hapa wala haitatulizwa. Lakini kumhusu mfalme wa Yuda, aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli juu ya maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia uliposikia maneno yangu dhidi ya mahali hapa, na dhidi ya wakazi wake, na umejinyenyekesha mbele yangu, nami pia nimekusikia. Adhabu ambayo nitailetea Yerusalemu, sitaileta wakati wa uhai wako. Utawala wako utakuwa wa amani.’” Basi, wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi. Kisha mfalme Yosia aliita na kukusanya viongozi wote wa Yuda na Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na wanaume wote wa Yuda, na wakazi wa Yerusalemu wakifuatana na makuhani, Walawi na watu wengine wote wakubwa kwa wadogo. Ndipo alipowasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme alisimama mahali pake akafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho. Tena aliwafanya wote waliokuwa katika Yerusalemu na katika Benyamini kuzingatia agano. Nao wakazi wa Yerusalemu waliishi kwa kufuata agano la Mungu, Mungu wa babu zao. Kisha Yosia aliondoa sanamu zote za kuchukiza zilizokuwa katika eneo lote la watu wa Israeli, na kuwahimiza watu wote wa Israeli kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Katika maisha yake yote hawakumwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.
2 Mambo ya Nyakati 34:19-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya torati, aliyararua mavazi yake. Mfalme akawaamuru Hilkia, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Abdoni, mwana wa Mika, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, kusema, Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa hao waliosalia wa Israeli na wa Yuda, kuhusu habari za maneno ya kitabu kilichoonekana; maana ghadhabu ya BWANA ni nyingi iliyomwagika juu yetu, kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la BWANA, kutenda sawasawa na yote yaliyoandikwa kitabuni humo. Basi Hilkia, na hao waliotumwa na mfalme, wakamwendea Hulda, nabii mwanamke, mkewe Shalumu, mwana wa Tohathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi; (naye alikuwa akikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili); wakasema naye kama hayo. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu, BWANA asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakazi wake, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda; kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike. Lakini kwa mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kuhusu uliyoyasikia, kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakazi wake, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA. Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari. Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda mfalme nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya Kitabu cha Agano kilichoonekana nyumbani mwa BWANA. Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo. Akawafanya wote walioonekana katika Yerusalemu na Benyamini walikubali. Na wenyeji wa Yerusalemu wakafanya kulingana na agano la Mungu, Mungu wa baba zao. Naye Yosia akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi zote zilizokuwa milki ya wana wa Israeli, akawafanya wote walioonekana katika Israeli kutumika, naam, wamtumikie BWANA, Mungu wao. Siku zake zote hawakuacha kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.
2 Mambo ya Nyakati 34:19-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme aliposikia yale maneno ya Sheria, akayararua mavazi yake. Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme, “Nendeni mkamuulize BWANA kwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki walioko Israeli na Yuda kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya BWANA ni kubwa mno ambayo imemwagwa juu yetu kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la BWANA wala hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.” Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili. Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, laana zote zilizoandikwa ndani ya hicho kitabu ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kunighadhibisha kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa juu ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza BWANA, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli kuhusu maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema BWANA. Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ” Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake. Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa BWANA pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, watu wote, wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya Agano mbele za BWANA ili kumfuata BWANA na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na ili kuyatii maneno ya Agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo Agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata Agano la BWANA, Mungu wa baba zao. Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka nchi yote iliyokuwa mali ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuwako katika Israeli wamtumikie BWANA Mungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.