Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 34:19-33

2 Nyakati 34:19-33 NEN

Mfalme aliposikia yale maneno ya Sheria, akayararua mavazi yake. Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme, “Nendeni mkamuulize BWANA kwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki walioko Israeli na Yuda kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya BWANA ni kubwa mno ambayo imemwagwa juu yetu kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la BWANA wala hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.” Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili. Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, laana zote zilizoandikwa ndani ya hicho kitabu ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kunighadhibisha kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa juu ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza BWANA, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli kuhusu maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema BWANA. Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ” Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake. Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa BWANA pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, watu wote, wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya Agano mbele za BWANA ili kumfuata BWANA na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na ili kuyatii maneno ya Agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo Agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata Agano la BWANA, Mungu wa baba zao. Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka nchi yote iliyokuwa mali ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuwako katika Israeli wamtumikie BWANA Mungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.