2 Mambo ya Nyakati 34:19-33
2 Mambo ya Nyakati 34:19-33 BHN
Mfalme aliposikia maneno ya sheria alirarua mavazi yake. Ndipo alipomwamuru Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, katibu Shafani na Asaya, mtumishi wa mfalme, akisema, “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu ambao wamebaki katika Israeli na Yuda, kuhusu maneno yaliyomo katika kitabu kilichopatikana. Kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imetuangukia, maana babu zetu hawakushika neno la Mwenyezi-Mungu, wala kufanya yaliyoandikwa humo.” Kwa hiyo Hilkia pamoja na wale wengine mfalme aliowatuma walimwendea nabii Hulda, mkewe Shalumu, mwana wa Tokathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi yaliyotumika hekaluni (alikuwa anaishi Yerusalemu katika mtaa wa pili); nao walizungumza naye juu ya mambo yaliyotokea. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambie huyo aliyewatuma kwangu, Mwenyezi-Mungu anasema hivi, ‘Tazama nitaleta uovu juu ya Yerusalemu na juu ya wakazi wake, laana zote zilizoandikwa katika kitabu kilichosomwa mbele ya mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukizia miungu mingine ubani ili wanikasirishe sana kwa kazi zote za mikono yao, basi ghadhabu yangu itamwagika juu ya mahali hapa wala haitatulizwa. Lakini kumhusu mfalme wa Yuda, aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli juu ya maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia uliposikia maneno yangu dhidi ya mahali hapa, na dhidi ya wakazi wake, na umejinyenyekesha mbele yangu, nami pia nimekusikia. Adhabu ambayo nitailetea Yerusalemu, sitaileta wakati wa uhai wako. Utawala wako utakuwa wa amani.’” Basi, wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi. Kisha mfalme Yosia aliita na kukusanya viongozi wote wa Yuda na Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na wanaume wote wa Yuda, na wakazi wa Yerusalemu wakifuatana na makuhani, Walawi na watu wengine wote wakubwa kwa wadogo. Ndipo alipowasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme alisimama mahali pake akafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho. Tena aliwafanya wote waliokuwa katika Yerusalemu na katika Benyamini kuzingatia agano. Nao wakazi wa Yerusalemu waliishi kwa kufuata agano la Mungu, Mungu wa babu zao. Kisha Yosia aliondoa sanamu zote za kuchukiza zilizokuwa katika eneo lote la watu wa Israeli, na kuwahimiza watu wote wa Israeli kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Katika maisha yake yote hawakumwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.