Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 3:16-28

1 Wafalme 3:16-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili. “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.” Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.” Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme. Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ” Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.” Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!” Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.” Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.

1 Wafalme 3:16-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni. Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani. Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu. Halafu, usiku mmoja, mtoto wake alifariki kwa sababu alimlalia. Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu. Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme. Ndipo mfalme Solomoni akasema, “Kila mmoja wenu anadai kwamba, mtoto wake ndiye aliye hai na kwamba aliyekufa si wake.” Basi, mfalme akaagiza: “Nileteeni upanga!” Wakamletea mfalme upanga. Mfalme akasema: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, umpe mmoja nusu na mwingine nusu.” Yule mwanamke aliyekuwa mama yake huyo mtoto aliye hai alishikwa na huruma juu ya mwanawe, akamwambia mfalme, “Tafadhali mfalme, msimuue mtoto. Mpe mwenzangu huyo mtoto aliye hai, amchukue yeye.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “La! Mtoto asiwe wangu wala wake. Mkate vipande viwili.” Mfalme Solomoni akasema, “Usimuue mtoto! Mpe mwanamke wa kwanza amchukue, kwani yeye ndiye mama yake.” Watu wote wa Israeli waliposikia juu ya hukumu ya mfalme, walimwogopa, wakatambua kwamba alikuwa na hekima ya Mungu iliyomwezesha kutoa hukumu.

1 Wafalme 3:16-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nilizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu. Nilipoamka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe. Amekufa. Na asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme. Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme. Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu. Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake. Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.

1 Wafalme 3:16-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu. Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme. Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme. Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu. Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake. Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.