1 Wafalme 3:16-28
1 Wafalme 3:16-28 SRUV
Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nilizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu. Nilipoamka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe. Amekufa. Na asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme. Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme. Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu. Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake. Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.