1 Wafalme 3:16-28
1 Wafalme 3:16-28 NEN
Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili. “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.” Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.” Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme. Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ” Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.” Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!” Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.” Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.