1 Wakorintho 4:8-13
1 Wakorintho 4:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Haya! Mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tutawale pamoja nanyi. Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu. Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini nyinyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, nyinyi ni wenye nguvu. Nyinyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa. Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi. Tena twataabika na kufanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa, tunawatakia baraka; tukidhulumiwa, tunavumilia; tukisingiziwa, tunajibu kwa adabu. Mpaka sasa tumetendewa kama uchafu wa dunia; na kwa kila mtu sisi ni takataka!
1 Wakorintho 4:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tuko uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na kuwa duni ya vitu vyote hata sasa.
1 Wakorintho 4:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.
1 Wakorintho 4:8-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia. Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.