1 Wakorintho 4:8-13
1 Wakorintho 4:8-13 NENO
Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia. Kwa ajili ya Al-Masihi sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Al-Masihi. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. Hadi saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki; tunapoteswa, tunastahimili; tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Hadi sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.