Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wimbo Ulio Bora 4

4
Bwana arusi
1Hakika u mzuri ewe mpenzi wangu,
hakika u mzuri!
Macho yako ni kama ya hua
nyuma ya shela lako,
nywele zako ni kama kundi la mbuzi
washukao katika milima ya Gileadi.
2Meno yako ni kama kondoo majike waliokatwa manyoya
wanaoteremka baada ya kuogeshwa.
Kila mmoja amezaa mapacha,
na hakuna yeyote aliyefiwa.
3Midomo yako ni kama utepe mwekundu,
kinywa chako chavutia kweli.
Nyuma ya shela lako,
mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga.
4Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,
uliojengwa ili kuhifadhia silaha,#4:4 uliojengwa … silaha: Makala katika Kiebrania si dhahiri.
ambako zimetundikwa ngao elfu moja
zote zikiwa za mashujaa.
5Matiti yako ni kama paa mapacha,
ambao huchungwa penye yungiyungi.
6Nitakaa kwenye mlima wa manemane,
na kwenye kilima cha ubani,
hadi hapo kutakapopambazuka,
na giza kutoweka.
7Tazama ulivyo mzuri ee mpenzi wangu,
wewe huna kasoro yoyote.
8Njoo, bibiarusi wangu tuondoke Lebanoni;
na tuiachilie mbali Lebanoni.
Shuka toka kilele cha mlima Amana,
toka kilele cha Seniri na Hermoni,
toka mapango ya simba,
toka milima ya chui.
9Umefurahisha moyo wangu, dada yangu, bi arusi,
umefurahisha moyo wangu,
kwa kunitupia jicho mara moja tu,
na kwa huo mkufu wako shingoni.
10Dada yangu, bi arusi;
pendo lako ni tamu ajabu.
Ni bora kuliko divai,
marashi yako yanukia kuliko viungo vyote.
11Midomo yako yadondosha asali, ee bibiarusi wangu;
ulimi wako una asali na maziwa.
Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ya Lebanoni.
12Dada yangu, naam, bi arusi,
ni bustani iliyofichika,
bustani iliyosetiriwa;
chemchemi iliyotiwa mhuri.
13Machipukizi yako ni bustani ya mikomamanga
pamoja na matunda bora kuliko yote,
hina na nardo.
14Nardo na zafarani, mchai na mdalasini
manemane na udi,
na mimea mingineyo yenye harufu nzuri.
15U chemchemi ya bustani,
kisima cha maji yaliyo hai,
vijito vitiririkavyo kutoka Lebanoni.
Bibi arusi
16Vuma, ewe upepo wa kaskazi,
njoo, ewe upepo wa kusi;
vumeni juu ya bustani yangu,
mlijaze anga kwa manukato yake.
Mpenzi wangu na aje bustanini mwake,
ale matunda yake bora kuliko yote.

Iliyochaguliwa sasa

Wimbo Ulio Bora 4: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia