Ufunuo 15:1-8
Ufunuo 15:1-8 BHN
Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa. Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Nguvu, matendo yako ni makuu na ya ajabu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.” Baada ya hayo nikaona hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ya kuwapo kwa Mungu. Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa na kanda za dhahabu vifuani mwao. Kisha, mmojawapo wa wale viumbe wanne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia hekaluni mpaka mwisho wa mabaa saba ya wale malaika saba.