Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 15:1-8

Ufunuo 15:1-8 NEN

Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika. Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu. Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: “BWANA Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu na ya ajabu. Njia zako wewe ni za haki na za kweli, Mfalme wa nyakati zote! Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamedhihirishwa.” Baada ya haya nikatazama, nalo hekalu, la hema la Ushuhuda, lilikuwa limefunguliwa mbinguni. Ndani ya lile hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ingʼaayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao. Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele. Nalo lile hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.