Ufunuo 15:1-8
Ufunuo 15:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa. Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Nguvu, matendo yako ni makuu na ya ajabu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.” Baada ya hayo nikaona hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ya kuwapo kwa Mungu. Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa na kanda za dhahabu vifuani mwao. Kisha, mmojawapo wa wale viumbe wanne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia hekaluni mpaka mwisho wa mabaa saba ya wale malaika saba.
Ufunuo 15:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa. Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa; na wale malaika saba, wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung'aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu. Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele. Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, mpaka yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.
Ufunuo 15:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa. Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa; na wale malaika saba, wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung’aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu. Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele. Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, hata yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.
Ufunuo 15:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika. Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu. Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: “BWANA Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu na ya ajabu. Njia zako wewe ni za haki na za kweli, Mfalme wa nyakati zote! Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamedhihirishwa.” Baada ya haya nikatazama, nalo hekalu, la hema la Ushuhuda, lilikuwa limefunguliwa mbinguni. Ndani ya lile hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ingʼaayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao. Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele. Nalo lile hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.