Ufunuo 14:14-20
Ufunuo 14:14-20 BHN
Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.” Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa. Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!” Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu. Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilomita 300.