Ufunuo 14:14-20
Ufunuo 14:14-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.” Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa. Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!” Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu. Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilomita 300.
Ufunuo 14:14-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji la dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.
Ufunuo 14:14-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.
Ufunuo 14:14-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akaja kutoka hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.” Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa. Malaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.