Ufunuo 14:14-20
Ufunuo 14:14-20 SRUV
Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji la dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.