Zaburi 89:38-52
Zaburi 89:38-52 BHN
Lakini sasa ee Mungu, umemtupa na kumkataa, umejaa ghadhabu dhidi ya huyo uliyemweka wakfu. Umefuta agano ulilofanya na mtumishi wako; umeitupa taji yake mavumbini. Kuta zote za mji wake umezibomoa; ngome zake umezivunjavunja. Wote wapitao wanampokonya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. Maadui zake umewapa ushindi; umewafurahisha maadui zake wote. Silaha zake umezifanya butu; ukamwacha ashindwe vitani. Umemvua madaraka yake ya kifalme ukauangusha chini utawala wake. Umezipunguza siku za ujana wake, ukamfunika fedheha tele. Ee Mwenyezi-Mungu, utajificha hata milele? Hata lini hasira yako itawaka kama moto? Ukumbuke, ee Bwana, ufupi wa maisha yangu; kwamba binadamu uliyemuumba anaishi muda mfupi! Ni mtu gani aishiye asipate kufa? Nani awezaye kujiepusha na kifo? Ee Bwana, ziko wapi basi fadhili zako, ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? Ee Bwana, ukumbuke anavyotukanwa mtumishi wako, jinsi nivumiliavyo matusi ya wasiokujua. Ona wanavyomzomea, ee Mwenyezi-Mungu; jinsi wanavyomdhihaki mteule wako kila aendako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu milele! Amina! Amina!