Zaburi 89:38-52
Zaburi 89:38-52 NEN
Lakini wewe umemkataa, umemdharau, umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako. Umelikana agano lako na mtumishi wako, na umeinajisi taji yake mavumbini. Umebomoa kuta zake zote, na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu. Wote wapitao karibu wamemnyangʼanya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake, umewafanya watesi wake wote washangilie. Umegeuza makali ya upanga wake, na hukumpa msaada katika vita. Umeikomesha fahari yake, na kukiangusha kiti chake cha enzi. Umezifupisha siku za ujana wake, umemfunika kwa vazi la aibu. Hata lini, Ee BWANA? Utajificha milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini? Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka. Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu! Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo, au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi? Ee BWANA, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni, ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi? Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa, jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote, dhihaka ambazo kwazo adui zako wamenisimanga, Ee BWANA, ambazo kwazo wamesimanga kila hatua ya mpakwa mafuta wako. Msifuni BWANA milele! Amen na Amen.