Zaburi 89:38-52
Zaburi 89:38-52 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini sasa ee Mungu, umemtupa na kumkataa, umejaa ghadhabu dhidi ya huyo uliyemweka wakfu. Umefuta agano ulilofanya na mtumishi wako; umeitupa taji yake mavumbini. Kuta zote za mji wake umezibomoa; ngome zake umezivunjavunja. Wote wapitao wanampokonya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. Maadui zake umewapa ushindi; umewafurahisha maadui zake wote. Silaha zake umezifanya butu; ukamwacha ashindwe vitani. Umemvua madaraka yake ya kifalme ukauangusha chini utawala wake. Umezipunguza siku za ujana wake, ukamfunika fedheha tele. Ee Mwenyezi-Mungu, utajificha hata milele? Hata lini hasira yako itawaka kama moto? Ukumbuke, ee Bwana, ufupi wa maisha yangu; kwamba binadamu uliyemuumba anaishi muda mfupi! Ni mtu gani aishiye asipate kufa? Nani awezaye kujiepusha na kifo? Ee Bwana, ziko wapi basi fadhili zako, ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? Ee Bwana, ukumbuke anavyotukanwa mtumishi wako, jinsi nivumiliavyo matusi ya wasiokujua. Ona wanavyomzomea, ee Mwenyezi-Mungu; jinsi wanavyomdhihaki mteule wako kila aendako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu milele! Amina! Amina!
Zaburi 89:38-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi wako. Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umelinajisi taji lake na kulitupa chini. Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu. Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amedharauliwa na jirani zake; Umeutukuza mkono wa kulia wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia. Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani. Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini. Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu. Hadi lini, Ee BWANA? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hadi lini? Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu! Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu? Bwana, ziko wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? Ukumbuke, Ee Bwana, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi. Ambayo adui zako wamesimanga, Ee BWANA, Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako. Na ahimidiwe BWANA milele. Amina na Amina.
Zaburi 89:38-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini Wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi wako. Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umeinajisi taji yake na kuitupa chini. Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu. Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amekuwa laumu kwa jirani zake; Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia. Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani. Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini. Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu. Ee BWANA, hata lini? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto? Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu! Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu? Bwana, zi wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? Ee Bwana, ukumbuke, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi. Ambayo adui zako wamesimanga, Ee BWANA, Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako. Na ahimidiwe BWANA milele. Amina na Amina.
Zaburi 89:38-52 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini wewe umemkataa, umemdharau, umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako. Umelikana agano lako na mtumishi wako, na umeinajisi taji yake mavumbini. Umebomoa kuta zake zote, na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu. Wote wapitao karibu wamemnyangʼanya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake, umewafanya watesi wake wote washangilie. Umegeuza makali ya upanga wake, na hukumpa msaada katika vita. Umeikomesha fahari yake, na kukiangusha kiti chake cha enzi. Umezifupisha siku za ujana wake, umemfunika kwa vazi la aibu. Hata lini, Ee BWANA? Utajificha milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini? Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka. Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu! Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo, au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi? Ee BWANA, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni, ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi? Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa, jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote, dhihaka ambazo kwazo adui zako wamenisimanga, Ee BWANA, ambazo kwazo wamesimanga kila hatua ya mpakwa mafuta wako. Msifuni BWANA milele! Amen na Amen.