Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 71:1-24

Zaburi 71:1-24 BHN

Kwako ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama; kamwe usiniache niaibike! Kwa uadilifu wako uniokoe na kunisalimisha; unitegee sikio lako na kuniokoa! Uwe mwamba wangu wa kukimbilia usalama, ngome imara ya kuniokoa, kwani wewe ni mwamba na ngome yangu. Niokoe, ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu, kutoka makuchani mwa wabaya na wakatili. Maana wewe Bwana u tumaini langu; tegemeo langu ee Mwenyezi-Mungu, tangu ujana wangu; nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu, ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. Mimi nitakusifu wewe daima. Kwa wengi nimekuwa kioja, lakini wewe u kimbilio langu imara. Kinywa changu kimejaa sifa zako, na utukufu wako mchana kutwa. Wakati wa uzee usinitupe; niishiwapo na nguvu usiniache. Maana maadui zangu wanasema vibaya juu yangu; wanaovizia uhai wangu wanafanya mipango, na kusema: “Mungu amemwacha; mfuateni na kumkamata, kwani hakuna wa kumwokoa!” Usikae mbali nami, ee Mungu; uje haraka kunisaidia, ee Mungu wangu. Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa; wenye kutaka kuniumiza wapate aibu na fedheha. Lakini mimi nitakuwa na matumaini daima; tena nitakusifu zaidi na zaidi. Kinywa changu kitatamka matendo yako ya haki, nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu ijapokuwa hayo yanapita akili zangu. Nitataja matendo yako makuu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu; nitatangaza kuwa ndiwe mwadilifu peke yako. Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu; tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu. Usiniache, ee Mungu, niwapo mzee mwenye mvi, hata nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako. Nguvu na uadilifu wako, ee Mungu, vyafika mpaka mbingu za juu. Wewe umefanya mambo makuu mno. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena. Nitakusifu pia kwa kinubi, kwa sababu ya uaminifu wako, ee Mungu wangu; nitakuimbia sifa kwa zeze, ewe Mtakatifu wa Israeli. Nitapaza sauti kwa furaha, ninapokuimbia wewe sifa zako, na roho yangu itakusifu maana umeniokoa. Nitatamka uadilifu wako mchana kutwa, maana waliotaka kuniumiza wameaibishwa na kufedheheshwa.

Soma Zaburi 71

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha