Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 71:1-24

Zaburi 71:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu. Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu, Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu. Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu. Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa. Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache. Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana. Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya. Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake. Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako. Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe? Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Tokea pande za chini ya nchi. Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo. Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli. Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa. Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.

Shirikisha
Soma Zaburi 71

Zaburi 71:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwako ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama; kamwe usiniache niaibike! Kwa uadilifu wako uniokoe na kunisalimisha; unitegee sikio lako na kuniokoa! Uwe mwamba wangu wa kukimbilia usalama, ngome imara ya kuniokoa, kwani wewe ni mwamba na ngome yangu. Niokoe, ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu, kutoka makuchani mwa wabaya na wakatili. Maana wewe Bwana u tumaini langu; tegemeo langu ee Mwenyezi-Mungu, tangu ujana wangu; nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu, ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. Mimi nitakusifu wewe daima. Kwa wengi nimekuwa kioja, lakini wewe u kimbilio langu imara. Kinywa changu kimejaa sifa zako, na utukufu wako mchana kutwa. Wakati wa uzee usinitupe; niishiwapo na nguvu usiniache. Maana maadui zangu wanasema vibaya juu yangu; wanaovizia uhai wangu wanafanya mipango, na kusema: “Mungu amemwacha; mfuateni na kumkamata, kwani hakuna wa kumwokoa!” Usikae mbali nami, ee Mungu; uje haraka kunisaidia, ee Mungu wangu. Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa; wenye kutaka kuniumiza wapate aibu na fedheha. Lakini mimi nitakuwa na matumaini daima; tena nitakusifu zaidi na zaidi. Kinywa changu kitatamka matendo yako ya haki, nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu ijapokuwa hayo yanapita akili zangu. Nitataja matendo yako makuu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu; nitatangaza kuwa ndiwe mwadilifu peke yako. Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu; tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu. Usiniache, ee Mungu, niwapo mzee mwenye mvi, hata nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako. Nguvu na uadilifu wako, ee Mungu, vyafika mpaka mbingu za juu. Wewe umefanya mambo makuu mno. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena. Nitakusifu pia kwa kinubi, kwa sababu ya uaminifu wako, ee Mungu wangu; nitakuimbia sifa kwa zeze, ewe Mtakatifu wa Israeli. Nitapaza sauti kwa furaha, ninapokuimbia wewe sifa zako, na roho yangu itakusifu maana umeniokoa. Nitatamka uadilifu wako mchana kutwa, maana waliotaka kuniumiza wameaibishwa na kufedheheshwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 71

Zaburi 71:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniponye, Unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Ngome imara ya wokovu wangu. Maana wewe, Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu. Ee Mungu wangu, uniponye mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu na mdhalimu, Maana ndiwe tegemeo langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu. Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. Nimekuwa kifani kwa watu wengi, Lakini wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu. Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa. Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache. Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaotaka kuniua hushauriana. Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya. Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. Lakini mimi nitakutumainia daima, Nitaendelea kukusifu zaidi na zaidi. Lakini mimi nitakutumainia daima Na nitaendelea kukusifu zaidi na zaidi. Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako. Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe? Wewe, uliyetuonesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Kutoka katika vina virefu chini ya nchi. Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo. Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli. Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa. Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.

Shirikisha
Soma Zaburi 71

Zaburi 71:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee BWANA, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe. Kwa haki yako uniponye na kuniokoa, unitegee sikio lako uniokoe. Uwe kwangu mwamba wa kimbilio, mahali nitakapokimbilia kila wakati; toa amri ya kuniokoa, kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu. Ee Mungu wangu uniokoe kutoka kwenye mkono wa mwovu, kutoka kwenye makucha ya watu wabaya na wakatili. Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee BWANA Mwenyezi, tegemeo langu tangu ujana wangu. Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe, ulinitoa tumboni mwa mama yangu. Nitakusifu wewe daima. Nimekuwa kama kioja kwa wengi, lakini wewe ni kimbilio langu imara. Kinywa changu kimejazwa sifa zako, nikitangaza utukufu wako mchana kutwa. Usinitupe wakati wa uzee, wala usiniache nguvu zangu zinapopungua. Kwa maana adui zangu wananisengenya, wale wanaonivizia kuniua wafanya hila. Wanasema, “Mungu amemwacha, mkimbilieni mkamkamate, kwani hakuna wa kumwokoa.” Ee Mungu, usiwe mbali nami, njoo haraka kunisaidia, Ee Mungu wangu. Washtaki wangu na waangamie kwa aibu, wale wanaotaka kunidhuru na wafunikwe kwa dharau na fedheha. Lakini mimi, nitatumaini siku zote, nitakusifu zaidi na zaidi. Kinywa changu kitasimulia haki yako, wokovu wako mchana kutwa, ingawa sifahamu kipimo chake. Ee BWANA Mwenyezi, nitakuja na kutangaza matendo yako makuu, nitatangaza haki yako, yako peke yako. Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu, hadi leo ninatangaza matendo yako ya ajabu. Ee Mungu, usiniache, hata niwapo mzee wa mvi, mpaka nitangaze uwezo wako kwa kizazi kijacho, nguvu zako kwa wote watakaokuja baadaye. Ee Mungu, haki yako imefika juu katika mbingu, wewe ambaye umefanya mambo makuu. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Ingawa umenifanya nipate taabu, nyingi na chungu, utanihuisha tena, kutoka vilindi vya dunia utaniinua tena. Utaongeza heshima yangu na kunifariji tena. Ee Mungu wangu, nitakusifu kwa kinubi kwa ajili ya uaminifu wako; Ee Uliye Mtakatifu wa Israeli, nitakuimbia sifa kwa zeze. Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha ninapokuimbia sifa, mimi, ambaye umenikomboa. Ulimi wangu utasimulia matendo yako ya haki mchana kutwa, kwa maana wale waliotaka kunidhuru, wameaibishwa na kufadhaishwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 71

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha