Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 68:1-18

Zaburi 68:1-18 BHN

Mungu ainuka, na maadui zake watawanyika; wanaomchukia wakimbia mbali naye! Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, ndivyo anavyowapeperusha; kama nta inavyoyeyuka karibu na moto, ndivyo waovu wanavyoangamia mbele ya Mungu! Lakini waadilifu hufurahi ajapo Mungu, hushangilia na kuimba kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake; mtengenezeeni njia yake apandaye mawinguni. Jina lake ni Mwenyezi-Mungu; furahini mbele yake. Mungu akaaye mahali pake patakatifu, ni Baba wa yatima na mlinzi wa wajane. Mungu huwapa fukara makao ya kudumu, huwafungua wafungwa na kuwapa fanaka. Lakini waasi wataishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, uliposafiri kule jangwani, dunia ilitetemeka, mbingu zilitiririsha mvua; kwa kuweko kwako, Mungu wa Sinai, naam, kwa kuweko kwako, Mungu wa Israeli! Ee Mungu, uliinyeshea nchi mvua nyingi, uliiburudisha nchi yako ilipokuwa imechakaa. Watu wako wakapata humo makao; ukawaruzuku maskini kwa wema wako. Bwana alitoa amri, nao wanawake wengi wakatangaza habari: “Wafalme na majeshi yao wanakimbia ovyo!” Kina mama majumbani waligawana nyara, ingawa walibaki mazizini: Sanamu za njiwa wa madini ya fedha, na mabawa yao yanangaa kwa dhahabu. Mungu Mwenye Nguvu alipowatawanya wafalme huko, theluji ilianguka juu ya mlima Salmoni. Ewe mlima mrefu, mlima wa Bashani, ewe mlima wa vilele vingi, mlima wa Bashani! Mbona unauonea kijicho mlima aliochagua Mungu akae juu yake? Mwenyezi-Mungu atakaa huko milele! Akiwa na msafara mkubwa, maelfu na maelfu ya magari ya kukokotwa, Bwana anakuja patakatifuni pake kutoka Sinai. Anapanda juu akichukua mateka; anapokea zawadi kutoka kwa watu, hata kutoka kwa watu walioasi; Mwenyezi-Mungu apate kukaa huko.

Soma Zaburi 68