Zaburi 38:11-22
Zaburi 38:11-22 BHN
Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu, na jamaa zangu wanakaa mbali nami. Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao; wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza. Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu. Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii; nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu. Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, kama mtu asiye na chochote cha kujitetea. Lakini ninakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu. Nakuomba tu maadui wasinisimange, wasione fahari juu ya kuanguka kwangu. Karibu sana nitaanguka; nakabiliwa na maumivu ya daima. Naungama uovu wangu; dhambi zangu zanisikitisha. Maadui zangu hawajambo, wana nguvu; ni wengi mno hao wanaonichukia bure. Hao wanaonilipa maovu kwa wema wangu, wananipinga kwa sababu natenda mema. Usinitupe, ee Mwenyezi-Mungu; ee Mungu wangu, usikae mbali nami. Uje haraka kunisaidia; ewe Mwenyezi-Mungu, uliye wokovu wangu.