Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 27

27
Kwa Mungu kuna usalama
(Zaburi ya Daudi)
1Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu,
ni nani nitakayemwogopa?
Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu,
sitamwogopa mtu yeyote.
2Waovu wakinishambulia,
na kutaka kuniangamiza,
hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka.
3Hata jeshi likinizunguka,
moyo wangu hautaogopa kitu;
hata nikikabiliwa na vita,
bado nitakuwa na tumaini.
4Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu,
nalo ndilo ninalolitafuta:
Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu
siku zote za maisha yangu;
niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu,
na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake.
5Siku ya taabu atanificha bandani mwake;
atanificha katika hema lake,
na kunisalimisha juu ya mwamba.
6Nami kwa fahari nitaangalia juu
ya maadui zangu wanaonizunguka.
Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake,
nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu.
Msaada wapatikana kwa Mungu
7Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia,
unionee huruma na kunijibu.
8Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!”#27:8 Njoo umtafute Mungu: Kiebrania: Utafute uso wangu, yaani kumwendea Mungu katika ibada na kumtegemea (taz pia 2Sam 21:1).
Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu.
9Usiache kuniangalia kwa wema.
Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;
wewe umekuwa daima msaada wangu.
Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu.
10Hata kama wazazi wangu wakinitupa,
Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake.
11Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu;
uniongoze katika njia iliyo sawa,
kwa sababu ya maadui zangu.
12Usiniache maadui wanitende wapendavyo;
maana mashahidi wa uongo wananikabili,
nao wanatoa vitisho vya ukatili.
13Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu
katika makao ya walio hai.
14Mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Uwe na moyo, usikate tamaa!
Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 27: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia