Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 105:1-45

Zaburi 105:1-45 BHN

Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake; yajulisheni mataifa mambo aliyotenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, miujiza yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake; Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, alimhakikishia Israeli agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu, tena walikuwa wageni nchini Kanaani. Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa; kutoka nchi moja hadi nchi nyingine. Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mungu alizusha njaa nchini mwao, akaharibu chakula chao chote. Lakini aliwatangulizia mtu mmoja, Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani. Walimfunga miguu kwa minyororo, na shingoni kwa nira ya chuma, Muda si muda alichotabiri kilitimia. neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti. Mfalme wa Misri akaamuru afunguliwe; mtawala wa mataifa akamwachilia huru. Alimweka kuwa mkurugenzi wa serikali yake, na mkuu wa mali yake yote; awaongoze maofisa wake apendavyo, na kuwafundisha wazee wake hekima. Ndipo Israeli akaingia nchini Misri; Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Mwenyezi-Mungu akawafanya watu wake wazae sana; akawajalia nguvu kuliko maadui zao. Aliwafanya Wamisri wawachukie watu wake, wakawatendea hila watumishi wake. Kisha akamtuma Mose mtumishi wake, akamtuma na Aroni mteule wake. Wakafanya ishara za Mungu kati ya Wamisri, na miujiza katika nchi hiyo ya Hamu. Mungu akaleta giza juu ya nchi; lakini Wamisri wakakataa kutii amri zake. Akageuza mito yao kuwa damu, akawaua samaki wao wote. Vyura wakaivamia nchi yao, hata jumba la mfalme likajawa nao. Mungu akanena, kukazuka makundi ya nzi, na viroboto katika nchi yote. Badala ya mvua akawapa mvua ya mawe, na umeme uliomulika nchi yao yote; akaharibu mizabibu na mitini yao, akaivunja pia miti ya nchi yao. Mungu akanena, kukazuka nzige, na panzi maelfu yasiyohesabika; wakaitafuna mimea yote katika nchi, wakayala mazao yao yote. Aliwaua wazaliwa wa kwanza nchini mwao, chipukizi wa kwanza wa jamaa za Wamisri. Kisha akawatoa watu wa Israeli nchini, wakiwa na fedha na dhahabu; wala hakuna hata mmoja wao aliyejikwaa. Wamisri walifurahia kuondoka kwao, kwani hofu iliwashika kwa sababu yao. Mungu alitandaza wingu juu ya watu wake, na moto ili kuwaangazia usiku. Waliomba naye akawaletea kware, akawapa mkate kutoka mbinguni kwa wingi. Alipasua mwamba maji yakabubujika; yakatiririka jangwani kama mto. Aliikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake. Basi akawatoa watu wake nchini, wateule wake wakaimba na kushangilia. Aliwapa nchi za mataifa mengine na kuwakabidhi mashamba ya wenyeji; kusudi watu wake watii masharti yake, na kufuata sheria zake. Asifiwe Mwenyezi-Mungu!

Soma Zaburi 105