Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 105:1-45

Zaburi 105:1-45 Biblia Habari Njema (BHN)

Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake; yajulisheni mataifa mambo aliyotenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, miujiza yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake; Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, alimhakikishia Israeli agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu, tena walikuwa wageni nchini Kanaani. Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa; kutoka nchi moja hadi nchi nyingine. Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mungu alizusha njaa nchini mwao, akaharibu chakula chao chote. Lakini aliwatangulizia mtu mmoja, Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani. Walimfunga miguu kwa minyororo, na shingoni kwa nira ya chuma, Muda si muda alichotabiri kilitimia. neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti. Mfalme wa Misri akaamuru afunguliwe; mtawala wa mataifa akamwachilia huru. Alimweka kuwa mkurugenzi wa serikali yake, na mkuu wa mali yake yote; awaongoze maofisa wake apendavyo, na kuwafundisha wazee wake hekima. Ndipo Israeli akaingia nchini Misri; Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Mwenyezi-Mungu akawafanya watu wake wazae sana; akawajalia nguvu kuliko maadui zao. Aliwafanya Wamisri wawachukie watu wake, wakawatendea hila watumishi wake. Kisha akamtuma Mose mtumishi wake, akamtuma na Aroni mteule wake. Wakafanya ishara za Mungu kati ya Wamisri, na miujiza katika nchi hiyo ya Hamu. Mungu akaleta giza juu ya nchi; lakini Wamisri wakakataa kutii amri zake. Akageuza mito yao kuwa damu, akawaua samaki wao wote. Vyura wakaivamia nchi yao, hata jumba la mfalme likajawa nao. Mungu akanena, kukazuka makundi ya nzi, na viroboto katika nchi yote. Badala ya mvua akawapa mvua ya mawe, na umeme uliomulika nchi yao yote; akaharibu mizabibu na mitini yao, akaivunja pia miti ya nchi yao. Mungu akanena, kukazuka nzige, na panzi maelfu yasiyohesabika; wakaitafuna mimea yote katika nchi, wakayala mazao yao yote. Aliwaua wazaliwa wa kwanza nchini mwao, chipukizi wa kwanza wa jamaa za Wamisri. Kisha akawatoa watu wa Israeli nchini, wakiwa na fedha na dhahabu; wala hakuna hata mmoja wao aliyejikwaa. Wamisri walifurahia kuondoka kwao, kwani hofu iliwashika kwa sababu yao. Mungu alitandaza wingu juu ya watu wake, na moto ili kuwaangazia usiku. Waliomba naye akawaletea kware, akawapa mkate kutoka mbinguni kwa wingi. Alipasua mwamba maji yakabubujika; yakatiririka jangwani kama mto. Aliikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake. Basi akawatoa watu wake nchini, wateule wake wakaimba na kushangilia. Aliwapa nchi za mataifa mengine na kuwakabidhi mashamba ya wenyeji; kusudi watu wake watii masharti yake, na kufuata sheria zake. Asifiwe Mwenyezi-Mungu!

Shirikisha
Soma Zaburi 105

Zaburi 105:1-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Haleluya. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote. Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtakeni BWANA na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka. Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa. Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni ndani yake, Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. Akaiita njaa iijilie nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea. Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani. Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma. Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya BWANA ilimjaribu. Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia. Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote. Awafunge masheki wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima. Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao. Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake. Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua. Akaweka mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu. Alituma giza, kukafunga giza, Wala hawakuyaasi maneno yake. Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawafisha samaki wao. Nchi yao ilijaa vyura, Vyumbani mwa wafalme wao. Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa mipakani mwao mwote. Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na moto wa miali katika nchi yao. Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya mipaka yao. Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika; Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao. Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao. Akawatoa hali wana fedha na dhahabu, Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa. Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia. Alitandaza wingu liwe funiko, Na moto utoe nuru usiku. Walipotaka akaleta kware, Akawashibisha chakula cha mbinguni. Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita pakavuni kama mto. Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Ibrahimu, mtumishi wake. Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha. Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu; Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya.

Shirikisha
Soma Zaburi 105

Zaburi 105:1-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Haleluya. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Yasimulieni maajabu yake yote. Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtafuteni BWANA na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote. Yakumbukeni matendo yake ya ajabu aliyoyafanya, Miujiza yake na hukumu alizotoa. Enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Hukumu zake ziko duniani kote. Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Abrahamu, Na ahadi yake kwa Isaka. Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Kama fungu la urithi wenu. Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni katika nchi, Wakatangatanga toka taifa hadi taifa, Toka ufalme mmoja hadi kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. Akasababisha njaa katika nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea. Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani. Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma. Hadi wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya BWANA ilimjaribu. Mfalme alituma watu na kumfungua, Mkuu wa watu akamwachilia huru. Akamweka kuwa mkuu wa nyumba yake, Na mwenye mamlaka juu ya mali yake yote. Awaongoze maofisa wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima. Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao. Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake. Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua. Akatenda mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu. Alituma giza, na kufanya nchi kuwa na giza, Wakayaasi maneno yake. Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawaua samaki wao. Nchi yao ilijaa vyura, Hata nyumbani mwa wafalme wao. Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa katika nchi yao yote. Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na umeme uliomulika ghafla katika nchi yao. Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya nchi yao. Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika; Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao. Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao. Akawatoa wakiwa na fedha na dhahabu, Katika makabila yao asiwepo mwenye kujikwaa. Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia. Alitandaza wingu liwe kifuniko, Na moto ili uwaangazie usiku. Walimwomba naye akaleta kware, Na kuwashibisha chakula cha mbinguni. Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita jangwani kama mto. Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Abrahamu, mtumishi wake. Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha. Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu; Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya.

Shirikisha
Soma Zaburi 105

Zaburi 105:1-45 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake, wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda. Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa, waambieni matendo yake yote ya ajabu. Lishangilieni jina lake takatifu, mioyo ya wale wamtafutao BWANA na ifurahi. Mtafuteni BWANA na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote. Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka, enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye ndiye BWANA Mungu wetu, hukumu zake zimo duniani pote. Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu, agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki. Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele: “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.” Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake, walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine. Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema: “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.” Akaiita njaa juu ya nchi na kuharibu chakula chao chote, naye akatuma mtu mbele yao, Yosefu, aliyeuzwa kama mtumwa. Walichubua miguu yake kwa minyororo, shingo yake ilifungwa kwa chuma, hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia, hadi neno la BWANA lilipomthibitisha. Mfalme alituma watu wakamfungua, mtawala wa watu alimwachia huru. Alimfanya mkuu wa nyumba yake, mtawala juu ya vyote alivyokuwa navyo, kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo na kuwafundisha wazee wake hekima. Kisha Israeli akaingia Misri, Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu. BWANA aliwafanya watu wake kuzaana sana, akawafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao, ndiye aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake, wakatenda hila dhidi ya watumishi wake. Akamtuma Mose mtumishi wake, pamoja na Aroni, aliyemchagua. Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao, miujiza yake katika nchi ya Hamu. Alituma giza na nchi ikajaa giza, kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake? Aligeuza maji yao kuwa damu, ikasababisha samaki wao kufa. Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao. Alisema, yakaja makundi ya mainzi, na viroboto katika nchi yao yote. Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe, yenye umeme wa radi nchini yao yote, akaharibu mizabibu yao na miti ya tini, na akaangamiza miti ya nchi yao. Alisema, nzige wakaja, tunutu wasio na idadi, wakala kila jani katika nchi yao, wakala mazao ya ardhi yao. Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao, matunda ya kwanza ya ujana wao wote. Akawatoa Israeli katika nchi wakiwa na fedha na dhahabu nyingi, wala hakuna hata mmoja kutoka kabila zao aliyejikwaa. Misri ilifurahi walipoondoka, kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia. Alitandaza wingu kama kifuniko, na moto kuwamulikia usiku. Waliomba, naye akawaletea kware, akawashibisha kwa mkate wa mbinguni. Alipasua mwamba, maji yakabubujika, yakatiririka jangwani kama mto. Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake. Aliwatoa watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za shangwe, akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali wengine walikuwa wameitaabikia: alifanya haya ili wayashike mausia yake na kuzitii sheria zake.

Shirikisha
Soma Zaburi 105

Zaburi 105:1-45

Zaburi 105:1-45 BHNZaburi 105:1-45 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima