Zaburi 10:1-18
Zaburi 10:1-18 BHN
Ee Mwenyezi-Mungu, mbona wasimama mbali? Kwa nini wajificha wakati tumo taabuni? Kwa kiburi waovu wanawatesa maskini; njama zao ziwanase wao wenyewe. Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya, mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu. Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.” Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.” Njia za mwovu hufanikiwa daima; kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake, na huwadharau maadui zake wote. Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi; sitapatwa na dhiki maishani.” Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma; mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu. Hujificha vijijini huku anaotea, amuue kwa siri mtu asiye na hatia. Yuko macho kumvizia mnyonge; huotea mafichoni mwake kama simba. Huvizia apate kuwakamata maskini; huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua. Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini; huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu. Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau; ameficha uso wake, haoni kitu!” Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu; usiwasahau wanaodhulumiwa. Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau, na kusema ati hutamfanya awajibike? Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima. Uzivunje nguvu za mtu mwovu; ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena. Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele! Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake. Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge; wampa moyo na kumtegea sikio. Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa, binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.