Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 10:1-18

Zaburi 10:1-18 SRUV

Ee BWANA, kwa nini wasimama mbali? Kwani unajificha nyakati za shida? Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza. Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana BWANA na kumdharau. Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Mungu Hatapatiliza. Mawazo yake yote ni, Hakuna Mungu; Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awakaripia. Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni. Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, Hujificha na kuotea vijijini. Katika maficho humwua asiye na hatia, Macho yake humtazama kisiri mtu duni. Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Na kumkokota akiwa wavuni mwake. Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe. Inuka, Ee Mungu BWANA, uuinue mkono wako, Ee Mungu Usiwasahau wanyonge. Kwa nini mdhalimu amdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza? Umeona, maana unaangalia matatizo na dhiki, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima. Uuvunje mkono wa mdhalimu, Na mwovu, uipatilize dhuluma yake, hadi usiione. BWANA ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa yataangamia kutoka nchi yake. BWANA, utayasikia matakwa ya wanyonge, Uutaidhibiti mioyo yao, utalitega sikio lako. Ili kumhukumu yatima na aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.

Soma Zaburi 10