Methali 30:15-33
Methali 30:15-33 BHN
Mruba anao binti wawili wasemao, “Nipe, nipe!” Kuna vitu vitatu ambavyo kamwe havishibi, naam, vitu vinne visivyosema, “Imetosha!” Kuzimu, tumbo la mwanamke lisilozaa, ardhi isiyoshiba maji, na moto usiosema, “Imetosha!” Kama mtu akimdhihaki baba yake, na kudharau utii kwa mama yake, kunguru wa bondeni watamdonoa macho, na kuliwa na tai. Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, naam, mambo manne nisiyoyaelewa: Njia ya tai angani, njia ya nyoka mwambani, njia ya meli baharini, na kinachomvuta mwanamume kwa mwanamke. Mwenendo wa mwanamke mwasherati ni hivi: Yeye hula, akajipangusa mdomo, na kusema, “Sijafanya kosa lolote!” Kuna mambo matatu ambayo huitetemesha dunia, naam, mambo manne ambayo haiwezi kuyastahimili: Mtumwa anayekuwa mfalme; mpumbavu anayeshiba chakula; mwanamke asiyependwa anayeolewa; na mjakazi achukuapo nafasi ya bibi yake. Kuna viumbe vinne vidogo sana duniani, lakini vina akili sana: Sisimizi: Wadudu wasio na nguvu, lakini hujihifadhia chakula wakati wa kiangazi; pelele: Wanyama wasio na uwezo, lakini hujitengenezea makao miambani; nzige: Hawana mfalme, lakini wote huenda pamoja kwa vikosi; mjusi: Waweza kumshika mkononi, lakini huingia katika ikulu. Kuna viumbe vitatu vyenye mwendo wa kupendeza, naam, kuna viumbe vinne vyenye mwendo mzuri; simba: Mnyama mwenye nguvu kuliko wote, wala hamwogopi mnyama mwingine yeyote; jogoo aendaye kwa maringo; tena beberu; na mfalme mbele ya watu wake. Kama umekuwa mpumbavu hata ukajisifu, au kama umekuwa unapanga maovu, chunga mdomo wako. Maana ukisukasuka maziwa utapata siagi, ukimpiga mtu pua atatoka damu; kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.