Mit 30:15-33
Mit 30:15-33 SUV
Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi! Kuzimu; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi! Jicho la mtu amdhihakiye babaye, Na kudharau kumtii mamaye; Kunguru wa bondeni wataling’oa, Na vifaranga vya tai watalila. Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, Naam, kuna manne nisiyoyafahamu. Mwendo wa tai katika hewa; Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba; Mwendo wa merikebu katikati ya bahari; Na mwendo wa mtu pamoja na msichana. Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu; Hula, akapangusa kinywa chake, Akasema, Sikufanya uovu. Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia. Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula; Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake. Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana. Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari. Wibari ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba. Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi. Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme. Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri. Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote; Jimbi aendaye tambo; na beberu; Na mfalme ambaye haasiki. Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako. Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.