Methali 17:1-28
Methali 17:1-28 BHN
Afadhali mkate mkavu kwa amani, kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi. Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu, atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo. Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya, mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake; anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao; watoto huwaonea fahari wazazi wao. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu, sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi! Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi; kila afanyacho hufanikiwa. Anayesamehe makosa hujenga urafiki, lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki. Onyo kwa mwenye busara lina maana, kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu; mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake. Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake, kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake. Mwenye kulipiza mema kwa mabaya, mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa; achana na ugomvi kabla haujafurika. Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatia yote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima, wakati yeye mwenyewe hana akili? Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote, ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu. Si jambo la akili kuweka rehani, na kuwa mdhamini wa mtu mwingine. Anayependa ugomvi anapenda dhambi; anayejigamba anajitafutia maangamizi. Mwenye moyo mpotovu hafanikiwi, na msema uongo hupatwa na maafa. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo mchangamfu ni dawa, bali moyo wenye huzuni hudhoofisha mwili. Mtu mbaya hupokea hongo kwa siri ili apate kupotosha haki. Mtu mwenye busara lengo lake ni hekima, lakini mpumbavu hupania kila kitu duniani. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na uchungu kwa mama yake mzazi. Si vizuri kumtoza faini mtu asiye na hatia; ni kosa kumchapa viboko muungwana. Asiyesema sana ana maarifa; mtu mtulivu ni mwenye busara. Hata mpumbavu akinyamaza huonekana ana hekima; akifunga mdomo wake huonekana kuwa mwenye akili.