Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 17:1-28

Methali 17:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Afadhali mkate mkavu kwa amani, kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi. Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu, atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo. Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya, mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake; anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao; watoto huwaonea fahari wazazi wao. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu, sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi! Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi; kila afanyacho hufanikiwa. Anayesamehe makosa hujenga urafiki, lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki. Onyo kwa mwenye busara lina maana, kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu; mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake. Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake, kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake. Mwenye kulipiza mema kwa mabaya, mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa; achana na ugomvi kabla haujafurika. Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatia yote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima, wakati yeye mwenyewe hana akili? Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote, ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu. Si jambo la akili kuweka rehani, na kuwa mdhamini wa mtu mwingine. Anayependa ugomvi anapenda dhambi; anayejigamba anajitafutia maangamizi. Mwenye moyo mpotovu hafanikiwi, na msema uongo hupatwa na maafa. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo mchangamfu ni dawa, bali moyo wenye huzuni hudhoofisha mwili. Mtu mbaya hupokea hongo kwa siri ili apate kupotosha haki. Mtu mwenye busara lengo lake ni hekima, lakini mpumbavu hupania kila kitu duniani. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na uchungu kwa mama yake mzazi. Si vizuri kumtoza faini mtu asiye na hatia; ni kosa kumchapa viboko muungwana. Asiyesema sana ana maarifa; mtu mtulivu ni mwenye busara. Hata mpumbavu akinyamaza huonekana ana hekima; akifunga mdomo wake huonekana kuwa mwenye akili.

Shirikisha
Soma Methali 17

Methali 17:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. Amchekaye maskini humtukana Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. Wana wa wana ndio taji la wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Sembuse midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye afichuaye siri hutenga rafiki. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. Afadhali mtu akutwe na dubu jike aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA. Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu. Asiye na hekima hupeana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini wa mtu mwingine. Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu. Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotovu huanguka katika misiba. Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa. Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu. Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia. Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa. Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si vyema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao. Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.

Shirikisha
Soma Methali 17

Methali 17:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. Wana wa wana ndio taji ya wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA. Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu. Aliyepungukiwa na akili hupana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini mbele ya mwenzake. Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu. Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotofu huanguka katika misiba. Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa. Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu. Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia. Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa. Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si kwema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao. Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.

Shirikisha
Soma Methali 17

Methali 17:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi. Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu. Kalibu ni kwa ajili ya fedha na tanuru ni kwa ajili ya dhahabu, bali BWANA huujaribu moyo. Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya; mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara. Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa. Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao. Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala! Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa. Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu. Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Mtu mbaya hupenda kuasi tu; mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake. Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, kuliko mpumbavu katika upumbavu wake. Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema, kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake. Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji; kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza. Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki, naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki: BWANA huwachukia sana wote wawili. Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu, wakati yeye hana haja ya kupata hekima? Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida. Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani, naye huweka dhamana kwa jirani yake. Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi; naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu. Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa; naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu. Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni; hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu. Moyo wenye furaha ni dawa nzuri, bali roho iliyopondeka hukausha mifupa. Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri ili kupotosha njia ya haki. Mtu wa ufahamu huitazama hekima, lakini macho ya mpumbavu huhangaika hadi kwenye miisho ya dunia. Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake na uchungu kwa yeye aliyemzaa. Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia, au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao. Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia, naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu. Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza, na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.

Shirikisha
Soma Methali 17