Mithali 17:1-28
Mithali 17:1-28 SRUV
Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. Amchekaye maskini humtukana Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. Wana wa wana ndio taji la wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Sembuse midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye afichuaye siri hutenga rafiki. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. Afadhali mtu akutwe na dubu jike aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA. Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu. Asiye na hekima hupeana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini wa mtu mwingine. Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu. Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotovu huanguka katika misiba. Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa. Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu. Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia. Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa. Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si vyema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao. Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.