Marko 14:12-26
Marko 14:12-26 BHN
Siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati ambapo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?” Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, na humo mtakutana na mwanamume mmoja anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema: Wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.” Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka. Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.” Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?” Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!” Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho. Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi. Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.” Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.