Marko 13:1-13
Marko 13:1-13 BHN
Yesu alipokuwa anatoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!” Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.” Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?” Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, kila mmoja akisema kuwa yeye ni mimi! Nao watawapotosha watu wengi. Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. “Lakini nyinyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, ili mpate kunishuhudia kwao. Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si nyinyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanawe; watoto nao watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.