Marko 13:1-13
Marko 13:1-13 SRUV
Alipokuwa akitoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, Mwalimu, tazama, yalivyo mawe na majengo haya! Yesu akajibu, akamwambia, Wayaona majengo haya makubwa? Halitabaki hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. Na alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, kuelekea hekalu Petro, na Yakobo, na Yohana, na Andrea walimwuliza kwa faragha, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya wakati, hayo yote yatakapokuwa karibu kutimia? Yesu akaanza kuwaambia, Jihadharini, mtu asiwadanganye. Wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye, nao watadanganya wengi. Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na mitetemeko ya ardhi mahali kwingi; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa uchungu. Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao. Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote. Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lolote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu. Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwaua. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hadi mwisho, ndiye atakayeokoka.