Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 4:1-13

Mika 4:1-13 BHN

Utakuja wakati ambapo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu utakuwa mkubwa kuliko milima yote. Naam, utakwezwa juu ya vilima vyote. Watu wengi watamiminika huko, mataifa mengi yataujia na kusema: “Twendeni juu kwenye mlima wa Mwenyezi-Mungu, twende katika nyumba ya Mungu wa Yakobo, ili atufundishe njia zake, nasi tufuate nyayo zake. Maana mwongozo utatoka huko Siyoni; neno la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu.” Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi, atakata mashauri ya mataifa makubwa ya mbali. Nayo yatafua mapanga yao kuwa majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea. Taifa halitapigana na taifa lingine, wala hayatafanya tena mazoezi ya vita. Kila mtu atakaa kwa amani chini ya mitini na mizabibu yake, bila kutishwa na mtu yeyote. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ametamka yeye mwenyewe. Mataifa mengine hufuata njia zao, kwa kuitegemea miungu yao, lakini sisi twafuata njia zetu kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, milele na milele. Mwenyezi-Mungu asema, “Siku ile nitawakusanya walemavu, naam, nitawakusanya waliochukuliwa uhamishoni, watu wale ambao niliwaadhibu. Hao walemavu ndio watakaobaki hai; hao waliochukuliwa uhamishoni watakuwa taifa lenye nguvu. Nami Mwenyezi-Mungu nitawatawala mlimani Siyoni, tangu wakati huo na hata milele.” Nawe kilima cha Yerusalemu, wewe ngome ya Siyoni, ambamo Mungu anafanya ulinzi juu ya watu wake, kama mchungaji juu ya kondoo wake; wewe utakuwa tena mji maarufu kama hapo awali, Yerusalemu utakuwa tena mji mkuu wa mfalme. Sasa kwa nini mnalia kwa sauti? Je, hamna mfalme tena? Mshauri wenu ametoweka? Mnapaza sauti ya uchungu, kama mama anayejifungua! Enyi watu wa Siyoni, lieni na kugaagaa kama mama anayejifungua! Maana sasa mtaondoka katika mji huu mwende kukaa nyikani, mtakwenda mpaka Babuloni. Lakini huko, mtaokolewa. Huko Mwenyezi-Mungu atawakomboa makuchani mwa adui zenu. Mataifa mengi yamekusanyika kuwashambulia. Yanasema: “Acheni mji wao utiwe najisi, nasi tuyaone magofu ya Siyoni!” Lakini wao hawafahamu mawazo ya Mwenyezi-Mungu wala hawaelewi mpango wake: Kwamba amewakusanya pamoja, kama miganda mahali pa kupuria. Mwenyezi-Mungu asema, “Enyi watu wa Siyoni, inukeni mkawaadhibu adui zenu! Nitawapeni nguvu kama fahali mwenye pembe za chuma na kwato za shaba. Mtawasaga watu wa mataifa mengi; mapato yao mtaniwekea wakfu mimi, mali zao mtanitolea mimi Bwana wa dunia yote.”

Soma Mika 4